Saturday, December 22, 2012

TUNAFANYA HIVI SI KWA KUJIFUARAHISHA BALI KUCHANGIA JITIHADA ZA WADAU WA MAENDELEO HAPA KARAGWE


                                            KKKT DAYOSISI YA KARAGWE
HOSPITALI TEULE YA WILAYA  – NYAKAHANGA

RISALA KWA MGENI RASMI  WAZIRI MKUU WA JAMUHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA KATIKA KILELE CHA JUBILEI YA MIAKA 100 YA HOSPITALI NYAKAHANGA TAREHE 02/09/2012.

Mheshimiwa, Mgeni rasmi,
Mheshimiwa Raisi Mstaafu, Dkt Benjami W. Mkapa
Mheshimiwa, Baba Askofu Dayosisi ya Karagwe,
Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera
Waheshimiwa wakuu wa wilaya kutoka mkoa wa Kagera,
Mh. Mkuu wa Wilaya ya Karagwe,
Mh. Makamu M/kiti wa Halmashauri ya wilaya, Karagwe
Mh. Mkurugenzi, halmashauri ya wilaya ya Karagwe
Waheshimiwa viongozi wa serikali,madhehebu ya dini,vyama vya siasa,taasisi na mashirika binafsi na ya umma,
Waheshimiwa wageni waalikwa, mabibi na mabwana.

1.      UTANGULIZI
Mheshimiwa Mgeni rasmi, jumuiya ya Nyakahanga hospitali inayoongozwa na  KKKT Dayosisi ya Karagwe kwa ushirikiano na serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tunapenda kukushukuru kwa dhati kukubali mwaliko wetu, na kuungana nasi katika siku hii ya kilele cha jubilei.

Mheshimiwa Mgeni rasmi, maadhimisho haya yanayofikia kilele chake leo tarehe 2/9/2012 yalianza tangu Jumapili ya tarehe 26/8/2012 kwa ibada maalum iliyofanyika hapa uwanjani na kuongozwa na Mhashamu Baba Askofu Dkt. Benson Bagonza na siku ya Jumatatu tarehe 27/8/2012 mpendwa wetu Mkuu wa Wilaya ya Karagwe Mh. Darry Ibrahim Rwegasira alizindua rasmi huduma zilizotolewa hapa uwanjani kwa juma nzima.

Mh. Mgeni rasmi, katika juma hili la maadhimisho hospitali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa ndani na nje ya nchi tumekuwa tukitoa huma bure za uchunguzi wa afya na ushauri wa kitaalam kwa wananchi waliotembela vibanda vilivoandaliwa.

Huduma zilizotolewa ni pamoja na:
Ø      Huduma za elimu ya afya
Ø      Huduma za uchunguzi wa magonjwa ya kisukari, moyo na shinikizo la damu
Ø      Huduma za upimaji wa virusi vya ukimwi
Ø      Huduma za elimu na uchunguzi wa saratani ya matiti
Ø      Uhamasishaji wa uchangiaji wa damu

Wananchi wengi wamepewa ushauri wa kitaalam juu ya afya zao na wale walioonekana kuhitaji tiba zaidi wameandikiwa kwenda sehemu husika kwa uchunguzi zaidi na tiba kama ifuatavyo:
·        General consultations       731
·        Diabetic clinic – klinik ya Kisukari    263
·        Upimaji wa VVU 2036   (66 sawa na asilimia 0.03 wamekutwa na maambukizi ya VVU, utaratibu wa kuwapatia huduma zaidi umeelekezwa kwao)
·        Waliochangia damu  19
·        Uzazi wa mpango  73
·        Upasuaji (surgeries)             14
·        Uchunguzi wa saratani ya matiti 108 ( kati ya hao 11 waligundulika kuwa na matatizo na kufanyiwa utaratibu ya uchunguzi zaidi, wengine wawili walikutwa na majibu na kufanyiwa upasuaji)

JUMLA YA WANANCHI WOTE WALIOPEWA HUDUMA KATIKA PANGO HUU MAALUM WA MAADHIMISHO YA MIAKA 100 NI 3134



Mheshimiwa, Mgeni rasmi, msingi wa huduma ya tiba katika hospitali ya Nyakahanga ulianzishwa na wamisionari kutoka Misioni ya Bethel,  Ujerumani. historia inaonesha kwamba  mwishoni mwa mwaka 1912 kituo kidogo cha tiba kilianzishwa hapa Nyakahanga.

Mheshimiwa mgeni rasmi, kituo hicho kwa wakati huo kilipitia misukosuko mingi ikiwemo kubadilika kwa utawala wa wakoloni kutoka kwa wajurumani kwenda kwa waingereza. Pia matukio ya vita kuu ya kwanza na ya pili ya dunia yaliathiri kwa kiasi kikubwa kituo hicho.

Athari hizo ni pamoja na kukatishwa kwa huduma kwa vipindi fulani lakini pia kuhama kwa kituo kwenye maeneo ya Bugene na Lukajange, kabla ya kurudishwa tena hapa Nyakahanga mwaka 1939 chini ya wamisionari waanzilishi.


Mwaka 1953,Kanisa la kiinjili la kilutheri lilichukua rasmi uendeshaji wa zahanati ya Nyakahanga toka kwa wamisionari ikiwa na uwezo wa kulaza wagonjwa wapatao 60 tu. Na mwaka huo huo kituo kilipandishwa hadhi na Hospitali. Mwaka 1953 – 1959 hospitali ilikuwa na majengo 3 na wagonjwa wachache. Zilikuwepo wodi mbili tu ambazo leo zinajulikana kama wodi B na C

Mnamo mwaka 1965 kulikuwa na haja ya Karagwe kuwa hospitali ya wilaya. Tarehe 11.2.1965 serikali iliandika barua kuleta maombi kwa Kanisa kuhusu Nyakahanga kufanya kazi kama hospitali ya wilaya. Ombi hilo lilikubaliwa na ndipo serikali na Kanisa waliingia kwenye makubaliano ya namna ya kuendesha hospitali hii ikiwa hospitali teule ya wilaya ya Karagwe.

Mh. Mgeni rasmi, Makubaliano hayo yalitaja wazi wajibu wa kila upande kuwa, Kanisa (KKKT) litakuwa mmiliki wa hospitali,kuajiri  watumishi,kutunza na kuendeleza majengo  (capital expenditure) na pia kusimamia uendeshaji wa shughuli za hospitali, Serikali kwa upande wake itawajibika kwa kutoa ruzuku ya mishahara kwa watumishi na pesa zote za uendeshaji wa Hospitali za siku kwa siku (recurrent expenditure).

Mheshimiwa Mgeni rasmi, huduma zitolewazo na hospitali hii ni pamoja na:
Ø      Huduma za wagonjwa wa nje.
Ø      Elimu na huduma ya afya ya msingi
Ø      Huduma za afya ya uzazi
Ø      Huduma ya wakinamama wajawazito na watoto
Ø      Huduma za upasuaji
Ø      Huduma na kinywa na meno
Ø      Hudma za macho
Ø      Huduma za afya ya akili – mental health
Ø      Huduma kwa walio na maambukizi ya VVU
Ø      Huduma za tiba shufaa (palliative care) na huduma majumbani kwa wagonjwa mahututi (homebased care)
Ø      Kliniki ya kisukari
Ø      Huduma za uchunguzi kwa mionzi  - diagnostic radiology
Ø      Uchunguzi wa njia ya chakula – endoscopy
Ø      Huduma za maabara


Mheshimiwa Mgeni rasmi, hospitali hii inao uwezo wa:
Ø      vitanda 224 vya kulaza wagonjwa,
Ø      wafanyakazi wa kudumu 254;
Ø      inahudumia wakazi zaidi ya 600,000 toka ndani na nje ya Karagwe.
Ø      Wastani wa wagonjwa wanaotibiwa kwa mwaka;-
o       Wagonjwa wa nje 35,000 – 40,000,
o       waliolazwa 11,000 – 13,000,
o        waliojifungua 3,500 – 4,000 na
o        wanaofanyiwa upasuaji 1,700 – 2,000.

Hospitali  hii inasimamia zahanati 4 ambazo zinamilikiwa na KKKT Dayosisi ya Karagwe.


2.      CHANGAMOTO.

1.   Watumishi.
Mheshimiwa Mgeni rasmi, pamoja na juhudi na kujitoa kwa watendakazi wa hospitali kuhudumia wananchi wenzao, watumishi hawa wanafanya kazi masaa mengi na kwa kwa kweli wengi wao huwa hawapati siku za mapumziko wanazozistahili. Hii inatokana na upungufu mkubwa wa watumishi hasa kwa kada za maafisa tabibu(waganga), wauguzi, wateknolojia na wateknolojia wasaidizi wa madawa, maabara, mionzi, watoa dawa ya usingizi na wafamasia.
Mh. Mgeni rasmi, katika hali kama hii, watumishi wa sekta hii ya afya wanahitaji motisha stahiki ili waweze kujitoa zaidi zaidi ya sasa katika kuhudumia jamii yenye uhitaji mkubwa wa huduma za afya na tiba.

Mh. Mgeni rasmi, urasimu na taratibu zinazobadilika badilika za ajira na kuingizwa watumishi kwenye payrol umekuwa kikwazo kikubwa kwa juhudi za uongozi wa hospitali kuajiri watumishi wanaohitajika.

Mh. Mgeni rasmi, watumishi waliowengi wa hospitali wanaishi kwa mashaka juu ya hatima ya mafao yao ya kustaafu lakini pia wapo ambao malipo yao ya mapunjo yamekuwa na usumbufu tangu mwaka 2008. Makato ya fedha zao kwa ajili ya pensheni yamekuwa na utata kwani imeonekana wengi wanakata fedha toka hazina Dar es salaam lakini haziwekwi kwenye akaunti zao za mifuko husika.

Mh. Mgeni rasmi, malalamiko ya watumishi katika sekta ya afya ni mengi, itoshe tu kusema kwamba watumishi wa hospitali ya Nyakahanga wana imani kubwa na serikali kuwa inayafanyia kazi.

Mh. Mgeni rasmi, kauli mbiu iliyochaguliwa na watendakazi wa hospitali ya Nyakahanga ni “shabaha yetu ni huduma bora za afya na tiba” 
Kauli mbiu hii mh. Mgeni rasmi itoshe kukuonyesha wewe, serikali yetu, viongozi wetu wa kanisa na umma wa watanzania kwamba tumejitoa kufanya kila lililo ndani ya uwezo wetu kufanikisha shabaha hii.

Mh. Mgeni rasmi, hata hivyo ikumbukwe kuwa watumishi wa sekta ya afya pia ni watu wenye majukumu ya kifamilia  na kimaendeleo binafsi, hivyo isichukuliwe tu kuwa hii ni kazi ya wito halafu mtu huyu akashindwa kulisha na kusomesha watoto wao. Maadhara ya baadaye kwa hali hii ni makubwa. Moja ni watu vijana wengi kukimbia masomo ya sayansi za tiba. Lakini pia mtumishi huyu pia atakaposhindwa kusomesha watoto wake ni fedheha kwa jamii na pia kuongeza vijana wasio na elimu kwenye taifa na hivyo kurudisha nyuma juhudi za maendeleo kitaifa.

Mh. Mgeni rasmi, changamoto hii ya watumishi ni kubwa na inaweze kuchukua siku nzima kuiongelea. Itoshe tu kutambua kwamba bila watumishi wa kutosha na tena wenye ari ya kazi, hata tungekuwa na majengo mazuri namna gani, hali ya huduma haitafikia malengo.

2.   Miundo mbinu.
Mheshimiwa  Mgeni rasmi, miundo mbinu mingi ni ya zamani hivyo inahitaji ukarabati au kupanuliwa. Upungufu uliopo hasa ni wa vyumba vya kulaza wagonjwa, vyumba vya ofisi za kufanyia kazi madaktari, nyumba za watumishi na uchakavu wa mfumo wa maji taka na umeme.

3.    Ruzuku 
Mheshimiwa Mgeni rasmi, fedha zinazotolewa kwa ajili ya ununuzi wa dawa na vifaa tiba toka serikalini ni kidogo, hazikidhi mahitaji. Hata zile zinazotolewa vifaa na madawa mara nyingi havipatikani toka kwa msambazaji mkuu aliyeidhinishwa na serikali. Fedha  pia zinazotolewa kama “OC” (other charges) ambayo hutumika pamoja na mambo mengine kugharimia matengenezo ya mitambo na gharama za umeme ni kidogo, ukilinganisha na makisio/mahitaji halisi











MAKISIO
HALISI
ASILIMIA
MAKISIO
HALISI
ASILIMIA

2009/2010
2009/2010
HALISI V.S
 2010/2011
2010/2011
HALISI V.S
MAPATO
TSHS.
TSHS.
MAKISIO
 TSHS
TSHS.
MAKISIO
Ruzuku toka Serikalini






      -Mishahara
   1,027,664,280.00
    662,634,700.00
64%
   991,103,531.60
  892,076,800.00
90%
      -Vifaa Tiba na Madawa  
      335,661,864.00
    178,795,996.09
53%
   360,222,482.40
  200,982,340.86
56%
     - Uendeshaji (OC)
      467,893,236.00
      23,911,972.00
5%
   545,948,724.90
    42,569,300.70
8%
 Mfuko wa pamoja (Busket Fund)
      237,285,000.00
    237,355,000.00
100%
   235,360,677.00
  235,360,677.00
100%
Vyanzo Vingine
      364,754,534.00
    352,015,641.40
97%
   276,900,000.00
  364,395,545.41
132%
Jumla ya Mapato
     2,433,258,914.00
   1,454,713,309.49
60%
  2,409,535,415.90
 1,735,384,663.97
72%







MATUMIZI






Mishahara
   1,027,664,280.50
    755,733,276.77
74%
   991,103,531.60
  897,751,989.50
91%
Vifaa Tiba na Madawa
        686,511,604.50
      291,307,609.00
42%
     694,594,831.90
     291,053,889.00
42%
Matumizi Mengine
        719,083,029.00
      413,630,427.68
58%
     723,837,052.40
     484,438,055.59
67%
Jumla ya Matumizi
     2,433,258,914.00
   1,460,671,313.45
60%
  2,409,535,415.90
 1,673,243,934.09
69%


4.   Mabadiliko ya mara kwa mara ya sera katika sekta ya Afya (Health Sector Reforms).
Mheshimiwa Mgeni rasmi, mabadiliko haya ya mara kwa mara ya sera ya Afya japo lengo lengo ni kuboresha huduma za afya na tiba, yameleta changamoto nyingi ndani ya hospitali.
Eidha kwa kutotolewa kwa ufafanuzi wa waraka ama kwa hospitali kutokuwezeshwa kutekeleza kikamilifu yaliyomo kwenye miongozo mbalimbali.
Mfano:              
·      Huduma kwa makundi maalum yenye msamaha
·      Sera ya uchangiaji wa huduma
·      Miongozo na taratibu za uapatikanaji wa madawa na vifaa tiba
Waraka wa posho za masaa ya ziada – kugawa watendakazi

5.   Maji:
Mh. Mgeni rasmi, hospitali ya Nyakahanga inakabiliwa na tatizo la upatikanaji wa maji ya uhakika. Jambo hili limekuwa mzigo kwa hospitali kwani huchangia kuongeza gharama za uendeshaji. Kwa mwezi hospitali hulipa kati ya Tsh 600,000 na 700,000 kama gharama za umeme kwa ajili ya mitambo ya kusukuma maji. Lakini pia tunakabiliwa na uchakavu wa mitambo hiyo inayohitaji ukarabati wa mara kwa mara na ni wa gharama.

Mh. Mgeni rasmi, hospitali inacho chanzo cha maji kwenye bonde la Nyakagera, hospitali ni miliki wa chanzo hicho na inalipa ada ya kila mwwaka kwwa mamlaka ya bonde la ziwa viktoria.
Mh. Mgeni rasmi  tatizo linalotukabili kwenye chanzo hiki ni kutishiwa usalama wa maji na pia kukauka kwani ujenzi wa nyumba za makazi karibu na chanzo hiki umeshika kasi kubwa.
Mh. Mgeni rasmi, suala la upatikanaji wa maji safi kwa matumizi ya majumbani ni tatizo kubwa hapa Karagwe. Hospitalini tumekuwa tukishuhudia madhara haya kwa kupokea wagonjwa wengi kutokana na kutumia maji yasiyo salama ikiwa wengine hata kupoteza maisha.
                 
                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                       
3.      MALENGO
Mheshimiwa Mgeni rasmi,tunapofikia miaka 100 ya kutoa huduma ya afya na tiba hapa Nyakahanga, Dayosisi ya Karagwe chini ya uongozi wake Baba Askofu Dkt Benson Bagonza, imejipanga kuhakikisha ile kauli mbiu yetu isemayo “shabaha yetu ni huduma bora za afya na tiba” inatimia siku si nyingi za usoni.

Mh. Mgeni rasmi, kama ulivyosikia, changamoto za kutoa huduma bora ni nyingi ila kanisa limejipanga kutafuta suluhu ya changamoto moja baada ya nyingine


Mh. Mgeni rasmi, moja ya mkakati wa kukomesha tatizo la uhaba wa  watumishi ni kuanzisha chuo cha sayansi za tiba na afya ambacho kitajumuisha shule za wauguzi, waganga, wateknologia wa maabara na maafisa afya.

Mh. Mgeni Rasmi, faida za Chuo hiki ni pamoja na:
a.      Kusaidia kupunguza upungufu wa wataalam  wa fani hizo hapa wilayani na nchini kwa ujumla.
b.      Kusaidia vijana wetu wanaomaliza elimu ya sekondari kupata elimu ya taaluma kwa gharama nafuu, zingatia mkoa hauna chuo cha waganga, ni gharama kubwa kwa wazazi kupeleka watoto wao nje ya mkoa kusomea taaluma hio.
c.      Chuo kitatoa nafasi nzuri kwa watumishi waliopo kazini kuweza kujiendeleza wakingali katika mazingira ya familia zao hivo kupunguza gharama na usumbufu wa kusomea nje.
d.      Chuo kitasaidia kuongeza ajira hivo kusaidia katika ukuaji wa uchumi wa mtu mmoja mmoja, familia na taifa kwa ujumla.


Mh. Mgeni rasmi, hospitali pia inayo mikakati ya kujenga uwezo katika maeneo yafuatayo:-
·  Kuendelea kujenga uwezo wa raslimali watu kwa njia ya mafunzo na ajira.
·  Kuboresha majengo ya hospitali kwa njia ya ukarabati na miundo mbinu ya kisasa kwa kujenga majengo mapya.
·  Kujenga na kuimarisha miradi endelevu.
·  Kujenga jamii ambayo ni mashahidi wa utukufu wa Mungu kwa njia ya injili.


4.      SHUKURANI
Mhe. Mgeni Rasmi, awali ya yote kwa niaba ya watendakazi wa hospitali teule ya Nyakahanga napenda kuchukua fursa hii kukushukuru wewe kwa kufika kwako katika kilele cha sherehe hizi za maadhimisho ya miaka 100 ya huduma hapa Nyakahanga

Shukurani za kipekee ziende kwa misioni ya Bethel nchini Ujerumani kwa uamuzi wao wa kuanzisha huduma za afya na tiba hapa Nyakahanga.

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa miongozo, ruzuku za mishahara, madawa na vifaa tiba na usimamizi.

Pia kwa maendeleo ya hospitali hii mpaka kufikia wafuatao ni kati ya wadau wakubwa na wanastahili shukurani zetu
·        Baba Askofu (mstaafu) Paul Mukuta
·        Baba Askofu (askofu)  Nelson Kazoba
·        Baba Askofu Dkt. Benson Bagonza
·        Mh. Balozi  Fredinand Ruhinda
·        Mh. Balozi Sir George Kahama
·        Halmashauri ya wilaya ya Karagwe
·        DANIDA
·        Church of Sweden
·        United Evangelical Mission
·        DMCDD
·        Dan Mission
·        Dan Church Aid
·        ATEGRIS



                                    
5.      HITIMISHO
Mheshimiwa  Mgeni rasmi, kama tulivyokwisha kusema hapo awali, dhumuni la maadhimisho ya jubilei ya miaka 100 ya  Hospitali ya Nyakahanga ni kutaka wananchi na wadau kufahamu hisoria ya hospitali hii, huduma tunazozitoa, changamoto zinazotukabili na pia malengo ya baadae ya hospitali katika juhudi zake za kutoa huduma kwa wananchi kwa kushirikiana na serikali.

Mheshimiwa Mgeni rasmi, tunapoanzisha chuo, kuna changamoto mbalimbali zinazohitaji nguvu ya pamoja kati ya Kanisa, Serikali, wadau wa ndani na nje na wananchi kwa ujumla. Kwa kuzingatia umuhimu wa chuo hiki katika jamii yetu, kupitia PPP (Public Private Partnership), tunaomba serikali itusaidie  yafuatayo:

-          Tamko la serikali juu ya umuhimu wa chuo hiki ni chachu inayhitajika kututia hamasa sisi na wadau wengine wa maendeleo
-          Serikali ipunguze urasimu katika usajili wa vyuo kama hivi, bila kushusha ubora.
-          Kama ilivyo kwa hospitali, serikali iwe mdau katika watakaofundisha katika chuo hiki

Mheshimiwa Mgeni rasmi, katika kutimiza malengo tumelenga kukusanya Tshs.1.8 bilioni mpaka sasa tumekwisha kukusanya 119,402,521, tunakushukuru wewe kwa kwa harambee uliyoiendesha kwa umahiri mkubwa hapo jana na kuweza kufikiwa kwa kiwango hicho.
                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                    
Mh. Mgeni rasmi, tunarudia kukushukuru kwa ujio wako  tukikuomba wewe pamoja na serikali kutuunga mkono katika juhudi hizi za kuhahkikisha huduma za afya na tiba zinakuwa bora huku tukiamini kwamba changamoto zote tulizozitaja na nyingine ulizojionea utaziwakilisha sehemu husika na kupatiwa ufumbuzi .


ASANTE SANA.

Imeandaliwa na kamati ya Historia

Na kusomwa na Dr. Andrew Cesari
Mfawidhi wa Hospitali
0762751335

Nyakahanga, 2/8/2012

No comments:

Post a Comment