Monday, October 1, 2012

HARAKATI NA JITIHADA KAMA HIZI ZINABIDI KUUNGWA MKONO NA KILA MMOJA WETU.

Na Mbeki Mbeki 
 Karagwe.
Katika  harakati za kupambana na changamoto zinazowakabili wanafunzi walio katika mazingira hatarishi  wanafunzi  175 Wilayani Karagwe wameweza  kulipiwa karo kutoka Karagwe Women Saccos (KAWOSA).
Akizungumza hivi karibuni na waandishi wa habari katika shule ya Sekondari Ihembe Meneja wa Saccos hiyo Goleth Elias alisema kuwa wamewalipia wanafunzi walio katika mazingira hatarishi kiasi cha shilingi Milioni 35,000,000/= kwa ajili ya kulipia karo.
Elias alisema kuwa wametoa fedha hizo ili kuwapunguzia makali ya madai waliyonayo na kuwapa moyo wa kuendelea na masomo yao ambapo alisema kuwa baadhi ya watoto hao ni yatima kutokana na wazazi kufa kwa kutokana na magonjwa mbalimbali ikiwemo ikimwi na wengine wakiwa na wazazi wasio na uwezo
.
Meneja wa Saccos hiyo alieleza kuwa wanafunzi hao wamekuwa wakikatisha masomo yao kutokana na kukosa mahitaji muhimu ya shule ikiwa ni pamoja na kalamu vitabu, karo na matumizi mengine ya lazima.
Alizitaja baadhi ya shule za sekondari ambazo zimenufaika na fedha hizo kuwa ni Ihembe, Rugu, Nyakasimbi, Nyakahanga, Bugene, Kayanga na Ndama na shule nyingine amezitaja kuwa ni Ruhicho, Kiruruma Kawela, Kyabalisa, Nyabiyonza na shule ya Sekondari Nono.
Aliongeza  kuwa kutokana na uwezo wa ofisi yake kuwa mdogo kila mwanafunzi amelipiwa shilingi 20,000/= ambapo pia mwaka jana walilipiwa mahitaji ya darasani kutoka kwenye chama chao cha akiba na mikopo.
Naye, mwenyekiti wa Saccos hiyo Safina Amrani amewataka wanawake wilayani humo kujiunga na saccos yao ili kuweza kuinua vipato vyao kiuchumi, kuwa ongezeko kubwa la wanachama litasaidia chama chao kuwa na uwezo mkubwa wa kukopesha na kutoa misaada kama hiyo.
Aidha amewashauri wanafunzi walio pata msaada wa kulipiwa karo  kutumia  fursa hiyo ili kuwawezesha kukomboa maisha yao kwa baadae.

Kwa upande wake, Mkuu wa shule ya Bugene Peter Mushumbusi ameipongeza  bodi ya Kawosa kwa msaada wanayoitoa kwa watoto walio katika mazingira magumu na kuyataka mashirika mengine kujitokeza kutoa huduma kama hiyo katika jamii.
Hata hivyo, amewataka wanafunzi walionufaika na fedha hizo kusoma kwa bidii ili baadae waweze kuwasaidia watoto wengine wenye hali kama hizo ambapo pia alisema waachane na makundi ya kihuni, ulevi, na uvutaji bangi kuwa yanaweza kuhatarisha maisha yao.

No comments:

Post a Comment