Monday, October 1, 2012

WALIOCHOMA MOTO BWENI LA SEKONDARI WATINGAMAHAKAMANI


Na:Mbeki Mbeki 
Ngara
Wanafunzi watatu  wa shule ya sekondari ya Mt Alfred ya Rulenge wilaya ya Ngara mkoani Kagera  wamefikiswa katika mahakama ya wilaya  hiyo  wakikabiliwa na tuhuma za kupanga njama na kuhusika kuchoma moto  mabweni mawili ya shule hiyo Agosti 23 mwaka huu.

Akisoma mashitaka ya wanafunzi hao mbele ya hakimu  mfawidhi wamahakama ya wilaya ya  Ngara  Juma Mpuya ,mwendesha mashitaka wa polisi Stividana Webiro aliwataja washitakiwa kuwa ni Gozibert Godwini ( 21),Wilikimuson Daudi ( 16) na Rameck Biswalo Gama (18 )wote wakiwa wanasoma kidato cha  pili na tatu katika shule hiyo.

Webiro alisema mnamo Agost 23 mwaka huu majira ya 2:30 usiku washitakiwa walichoma mabweni mawili ya Nkurumah katika  shule ya Sekondari  ya mt .Alfred Rulenge iliyoko wilayani humo na kuwasababishia wanafunzi wenzao kupata hasara mbalimbali  kwa kuunguliwa na magodoro,  mavazi, vitabu, vitanda na vifaa vinginevyo vya kujifunzia.
 
Katika kesi hiyo washitakiwa wote watatu walikana makosa hayo  na kurudishwa rumande hadi kesi hiyo itakapotajwa tena   September 18 mwaka huu
Aidha kufuatia tukio la kuunguzwa mabweni hayo kikao cha bodi ya shule hiyo kimefanyika na kubaini thamani ya  hasara  iliyojitokeza ambapo majengo ya shule ,mali za wanafunzi na mali nyinginezo vimekadiliwa kuwa na thamani ya shilingi milioni 200
 
Aidha Katibu wa bodi na ambaye ni mkuu wa shule ya sekondari ya mt Alfred Spriani Vumilia alisema  mara baada ya ya tukio hilo zilipelekwa taarifa wizara ya elimu na mafunzo ya ufundi uongozi wa wizara umeshauri mabweni hayo kujengwa upya na kuwekewa miundombinu ya usalama kwa wanafunzi.

“Kwa sasa tunasubiri kufanya uchambuzi wa vyanzo vya mapato na kutafuta wahisani au wafadhili wa shule ili kujenga mabweni mapya kama ilivyoshauri  wizara ya elimu na mafunzo ya ufundi”.Alisema Vumilia.

Kwa sasa wanafunzi wa kiume wa kidato cha pili na tatu waliounguliwa na mabweni wanasaidiwa na wazazi na wasamalia kupata mavazi na vifaa vya kujifunzia na wanaishi na wenzao katika mabweni mengine yaliyosalia kwa kulala wanafunzi wawili katika kitanda kimoja shuleni hapo.

No comments:

Post a Comment