Waathirika wa barabara ya Kyaka hadi Bugene yenye urefu wa kilomita 59.1 wameitaka serikali kuwalipa fidia ya makaburi 57 ambayo yalifukuliwa katika Kijiji cha Kishao bila fidia.
Hayo yalibainishwa jana na baadhi ya waathirika wa barabara hiyo inayojengwa kwa kiwango cha lami katika Mkutano wa hadhara katika kata ya Bugene, wilayani Karagwe.
Walisema kuwa malalamiko yao ya kuitaka serikalikuwalipia fidia ya makaburi hayo 57 ya jamaa zao waliokufa kati ya miaka 100 iliyopita walishayafikisha kwa Waziri wa ujenzi na miundombinu, waziri wa ardhi nyumba na maendeleo ya makazi na Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Jakaya Mrisho kati ya Januari na mei mwaka huu.
Walieleza kuwa waliamuliwa na wakala wa barabara mkoa wa Kagera (TANROADS) kuondoa, na kufukua makaburi bila fidia jambo ambalo walisema linawapelekea kutoiamini serikali yao katika kuwatendea haki.
Mmoja wa waathirika hao Adventina Furuka alisema kuwa alilazimika kufukua na kuhamisha makaburi manane bila fidia kutoka TANROAD ambapo aliongeza kuwa hata fidia walizopewa kwa baadhi ya waathirika hao katika mashamba na nyumba zilikuwa hazilingani na thamani ya mali zao.
Alisema kuwa baadhi yao hawakupewa kabisa fidia ya nyumba na mashamba ambapo barabara hiyo ndiyo iliyowavamia kwani kijiji hicho kimekuwepo tangu mwaka 1800.
Naye, Brighton Lwizah (85) alisema kuwa kwa kuwa serikali imeshindwa kuwalipa fidia za mali zao na kuunda tume ya kuchunguza malalamiko yao watakuwa tayari kupeleka malalamiko yao mahakamani, kuweka kizuizi (Cort injection) cha kuzuia ujenzi wa barabara kuendelea.
Lwizah aliongeza kuwa watakuwa tayari kuwakabidhi kadi za chama cha mapinduzi (CCM) kwa kuwa kimeshindwa kusimamia malalamiko yao na kuhakikisha fidia zao na stahiki zinapatikana.
Kwa upande wake Diwani wa kata hiyo Alstides Muliro amekiri kuyafahamu malalamiko hayo yanayowahusisha waathirika wapatao (85) wa barabara hiyo na kuwa suala hilo watalifikisha kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri, Serikali kuu, TANROAD mKOA NA Mkuu wa mkoa ili kulipatia ufumbuzi wa haraka kabla halijaleta madhara zaidi.
Aidha Walulya Sekweyama ambaye pia ni Katibu wa Waathirika hao alisema katika maongezi yake na Ofisi ya TANROAD Mkoa, na Mkuu wa Mkoa walihaidi kutatua mgogoro huo ndani ya siku 14, ambapo hadi sasa Ofisi hizo zinaendelea kupuuzia malalamiko hayo.
Hata hivyo alisema kuwa wataheshimu ushauri wa diwani wao kabla ya kupeleka mashtaka mahakamani ya kudai haki zao za msingi na kuwa hawata siri kufanya hivyo endapo majibu yatakayotolewa hawataridhika nayo.
No comments:
Post a Comment