Thursday, April 19, 2012

MSAKO WA WAFUGAJI HARAMU NGARA-KAGERA


Ng’ombe 400 kutoka Rwanda wakamatwa  wilayani Ngara

Na Shaaban Ndyamukama
Maofisa waandamizi wa halmashauriya wilaya ya Ngara Mkoani Kagera wamenusurika kuuawa na Kundi la wafugaji wanaodaiwa kutoka nchi jirani ya Rwanda wakati wa zoezi la kusaka Ng’ombe ambao hawajapigwa chapa ya alama ya Tanzaniawalioko wilayani humo





 BAADHI YA NG'OMBE WALIOKAMATWA KTK MSAKO HUO

Maofisa hao wa serikali walilazimika kutimua mbio kunusuru maisha yao baada ya wafugaji hao wanaoendesha shughuli zao katika pori la kimisi lililoko kwenye wilaya za  Ngara na Karagwe, kuwakimbiza huku wakiwa na bunduki aina ya SMG yenye magazini ya  risasi 30.

Tukio hilo limetokea jumamosi Machi 31 wakati maofisa hao wa serikali wakiongozwa na Afisa mifugo wa wilaya ya Ngara Dr Richard Ngowi na Afisa tafara ya Nyamiaga Bw Godian Bagambweki, wakifanya msako dhidi ya  mifugo iliyoko wilayani humo kinyume cha sheria

“Tulipofika katika kitongoji cha Kaumuli kata ta Kasulo, tulikamata kiasi cha ng’ombe 400 ambao wanasadikiwa kutoka nje ya nchi na ng’ombe hao ni mali ya Medard Muhutu Mudei raia kutoka Rwanda ambao tuliwakamata kwa kuwa hawana chapa inayowatambulisha kama Ng’ombe wa Tanzania. be 200”, alisema Dr Ngowi

Alisema wachungaji wa ng’ombe wengine 200 mali ya Bw Jackson Venant ambaye naye  anadaiwa kuwa mwenyeji wa Rwanda, walichuka silaha za ina mbalimbali ikiwa ni pamoja a bunduki aina ya SMG na kuanza kuwatishia

“Kundi la wachungaji wanaofikia 18, wakiwa na mapanga, marungu na Bunduki walianza kututishia, askari mgambo sita ambao walikuwa wamefuatana nasi bila silaha walianza kukimbia na sissi tukafuata”, Alisema Dr Ngowi

Alisema walilazimika kuacha ng’ombe hao na kwenda kuomba msaada kwa askari polisi walioko kwenye kizuizi cha barabara inayotoka Ngara kuelekea Karagwe, ambapo wachungaji hao walirejea porini baadaya kuwaona askari polisi.

Dr Ngowi amesema kwa mujibu wa sheria ya magonjwa ya mifugo namba 17 ya mwaka 2003, kila mmiliki anapaswa kutozwa faini isiyoipongua shilingi milioni mbili kwa kosa la kuingiza nchini mifugo ambayo haina chapa ya Tanzania.

Aidha amesema wamiliki hao wanapaswa kutozwa faini ya  shilingi elfu  50 kwa kila  ng’ombe kwa kuharibu mazingirra ya halmashauri husika

Kwa muda mrefu maeneo ya mapori ya wilaya za mkoa wa kagera yamevamiwa na wafugaji kutoka Rwanda na Burundi, maelfu ya mifugo na kusababisha madhara mbalimbali ikiwa ni pamoja a uharibifu wa mazingira
 Katika hatua nyingine Afisa tarafa ya Nyamiaga Bw Godian Bagambweki ambaye alishiriki katika msako huo wa ng’ombe amedai kushuhudia mizoga ya Tembo 12 katika pori la kimisi ambao waliuawa na watu wanaosadikiwa kuwa majangili ambao waliondoka na meno ya tembo hao

“Mizoga hiyo ya tembo nimeishuhudia jirani na zizi la Bw Jackson anayeishi kweye pori hilo. Kama serikali tunatakiwa kujipanga na kuchukua hatua zaidi dhidi ya watu wenye mifugo katika mapori ya hifadhi” .Alisema afisa tafara huyo

Mwezi June mwaka jana wakazi sita wa kijiji cha Murubanga wilayani Ngara wanadaiwa kuuawa na wafugaji kutoka nje ya nchi wakati wananchi hao wakipinga hatua ya ng’ombe wa wafugaji hao kulisha katika mashamba yao

Akizungumzia tukio hilo la siku hiyo Mkuu wa wilaya ya Ngara Kanali Mstaafu  ameliagiza jeshi la Polisi  kumtafuta na kumkamata mfugaji huyoJackson Venant  ili aweze kufikishwa kwenye mikono ya sheria

Akiongea katika eneo la Kata ya Kasulo baada ya kupata taarifa hizo, kanali Nyakonji alisema idara ya uhamiaji haina budi kufanya ufuatiliaji ili kubaini iwapo wafugaji hao wanaishi nchini kwa kufuata sheria

Katika mkutano wa bunge uliomalizika mwezi Februari mwaka huu  , wabunge wa mkoa huo kupitia kauli ya mbunge wa Muleba kaskazini charles Mwijage na Mbunge wa Karagwe Godbes waliitaka serikali kutoa tamko lini wahamiaji haramu na walio na mifugo wataondoka mkoani kagera kwa kuwa wanaharibu mazingira na kuhatarisha usalama wa raia na mali zao

Waziri wa mambo ya ndani Shamsi  Vuai Nahodha aliahidi kuchukua hatua dhidi ya watu wanaodaiwa kuingiza mifugo kutoka nchi jirani na kusababisha madhara mbalimbali mkoani humo baada ya kutoa agizo kwa kamati za ulinzi na usalama za wilaya zote  kuacha kutoa vibali kwa wahamiaji hao kupitia ngazi yoyote .

Kw amuda mrefu serikali imekuwa ikitoa ahadi za kuwaondoa wafugaji hao, kila mara  ambapo mwaka 2006 Rais Jakaya Kikwete aliagiza kuondolewa kwa wafugaji hao, lakini agizo hilo limeshindwa kutekelezwa

No comments:

Post a Comment