Saturday, May 12, 2012

MADIWANI WA CHADEMA WASUSIA KIKAO bIHARAMULO

MADIWANI wa halmashauri ya wilaya ya Biharamulo mkoani kagera wameweka kando tofauti zao za kisiasa na kulazimika kususia kikao cha baraza hilo kutokana na kumtuhumu mkurugenzi wa halmashauri hiyo Alhaji Zuber  Mbyana kupuuza maazimio ya vikao halali vya madiwani.
Hatua hiyo imetokana na taarifa iliyowasilishwa na diwani wa viti maalumu Ziyuni Hussen baada ya kutoa hoja ya kulitaka baraza hilo kususia kikao hicho kwa madai mkurugenzi wa halmashauri hiyo amekuwa akikaidi  kutekeleza mambo mbalimbali wanayoyaadhimia kwenye vikao vya baraza hilo na kwamba amekuwa akitekeleza mambo anayotaka yeye mwenyewe.
Baadhi ya mambo yaliyopelekea kususia kikao hicho ni pamoja na kutotekelezwa azimio la madiwani hao kwenda kutembelea  mgodi wa dhahabu wa TULAWAKA ili kujionea shughuli zinazofanywa na wawekezaji hao na kuwataka kulipa kwa wakati malipo ya  mrahaba wa kiasi cha shilingi 300 milioni kwa mwaka.
Mbali na hilo ni pamoja na kutaka kutembelea kwenye msitu wa hifadhi ya taita ya Burigi kwa lengo la kujionea uharibifu wa mazingira ambao umesababishwa na baadhi ya wahamiaji haramu kuweka makazi,mifugo,ukataji miti ya kupasua mbao,kilimo na uchomaji mkaa kinyume cha sheria.
Kutokana na hali hiyo walidai kushindwa kutekelezwa kwa maazimio hayo kunaonyesha wazi jinsi mkurugenzi  wao asivyokuwa makini  na utumishi wake na badala yake amekuwa akifanya kazi kwa mazoea hali inayopelekea baadhi ya madiwani kutokuwa na imani naye.
Katika kikao hicho ambacho kilidumu kwa takribani dakika 2 muda mchache baada ya kaimu mkurugenzi wa halmashauri hiyo  Zabron Njanga kusimama kwa lengo la kufungua kikao ambapo ilitolewa taarifa kutoka kwa diwani Hussen akimtaka mwenyekiti wa kikao hicho kusitisha baraza hilo kwa madai ya kutokuwa tayari kujadili ajenda mpya zilizowasilishwa mbele yao kingali maamuzi ya awali yakiwa hayajatekelezwa.
Hatua hiyo ilipelekea madiwani hao kuweka kando tofauti zao za kisiasa na kuungana kwa pamoja kususia baraza hilo huku wakionekana kutetea maamuzi hayo kwa madai litakuwa fundisho kwa viongozi  wengine kutekeleza maamuzi yanayotolewa na vikao halali vya madiwani.
Kaimu mwenyekiti wa halmashauri hiyo Laurent  Kakuru alisema hatua ya madiwani hao ilikuwa sahihi na kwamba anaungana na hoja za madiwani hao kutokana na maamuzi ya vikao kupuuzwa huku akiwatupia lawama baadhi ya watumishi wa halmashauri hiyo kujihusisha na mianya ya rushwa kinyume cha sheria.
“Hata mimi ninaungana na maamuzi ya madiwani wenzangu kwa kuwa mkurugenzi wetu amekuwa hatekelezi baadhi ya maamuzi yetu…kwani tuliomba kutembelea kwenye vivutio vya hifadhi ya taifa ya Burigi lakini hakuna majibu ya kulidhisha…pia tuliomba kutembelea mgodi wa dhahabu wa Tulawaka lakini bado suala hilo limekuwa kitendawili” alisema Kakuru
Kwa upande wake mnadhimu wa kambi ya upinzani ya madiwani wa chadema wilayani humo Josephat Kayamba ameupongeza uamuzi uliofikiwa na madiwani hao na kwamba hatua hiyo ni mwanzo mzuri kwa madiwani wa chama tawala kusimamia maamuzi yanayoamuliwa badala ya kuwa mashabiki wa kupinga hoja zinazoibuliwa na madiwani wa upinzani.
Alisema tamko la Chadema ni kuwa linamtaka mkurugenzi wa halmashauri hiyo kuitisha kikao cha baraza jingine ndani ya siku 21 ili waweze kutoa taarifa ya tume iliyoundwa kuchunguza ubadhilifu wa fedha za miradi ya maendeleo.
Aidha walionyesha kuwa na mashaka ya upatikanaji wa hati safi katika halmashauri yao na kulazimika kuhoji vigezo vinavyotumika kutokana na halmashauri hiyo kuwa ya mwisho katika ukusanyaji  mapato ya vyanzo vya ndani kwa kipindi cha robo tatu ya mwaka2011/2012 katika mkoa wa kagera.  
Akijibu tuhuma hizo kaimu mkurugenzi  huyo alikanusha vikali madai yaliyotolewa na madiwani kwa kuwa ofisi yake ilikuwa na majibu ya kutosha kuhusiana tuhuma zilizoelekezwa kwenye ofisi hiyo.

No comments:

Post a Comment