Sunday, March 17, 2013

WANAKARAGWE WAPEWA SOMO JUU YA WAJUMBE WA MABARAZA YA KATIBA



Na
     Juhudi  Felix
Karagwe
Wananchi,asasi za kiraia na wanaharakati wa kueneza elimu ya demokrasia nchini  wametakiwa kuungana kwa pamoja kwa ajili ya kuhakikisha wanapata wawakilishi wenye sifa stahili kwenye mabaraza ya mabadiliko ya  katiba.

Rai hiyo ilitolewa na Jimmy   Ruhende katika mkutano wa Katiba ni Yetu uliofanyika kwenye Ukumbi wa kituo cha Habari na Maarifa cha Karadea kilichopo mjini Kayanga.

Alisema kuwa ili kuhakikisha mchakato wa kujadili rasimu ya katiba mpya ni lazima kuwa na wajumbe wa mabaraza wa katiba ambao siyo mamuluki wa kupandikizwa na watu kwa maslahi yao binafsi au kundi fulani lenye maslahi yao binafsi.

Bwana Jimmy Ruhende ambaye ni mwezeshaji toka shirika la Action For Democracy  and Local Government linalojishughulisha  na mradi wa Katiba ni Yetu chini ya Forum Syd  Tanzania amesema kuwa endapo wanaharakati,asasi za Kiraia na wananchi kwa ujumla wasiposhiriki kikamilifu haitawezekana kuwa na katiba nzuri pia wajumbe wa mabaraza ya katiba kupitia rasimu hawatawasilisha vyema matakwa ya wananchi bali maslahi binafsi kwa matakwa yao na wafuasi wao.

Aidha,washiriki wa mkutano huo wameonesha kushangazwa na hatua ya kupokea barua za kuomba kuwa wajumbe wa mabaraza kuzungushwa kutokana na mkanganyiko wa haswa ni nani mhusika wa kupokea barua hizo haswa kwa walio kwenye mamlaka ya mji mdogo wa Kayanga,Bugene na Ihanda wameomba uongozi wa halmashauri kutoa maelekezo sahihi kuepusha wananchi kupoteza haki yao ya msingi.

Hata hivyo Bwana Ruhende amewataka wananchi wote vijana,wazee,wanaume na wanawake kuandika barua za kuomba kuwa wajumbe wa mabaraza ya katiba ili kushiriki kikamilifu na kuwa wamiliki wa katiba pia kusukuma Agenda zao walizonazo kwa manufaa ya maendeleo yao na Taifa kwa ujumla.

No comments:

Post a Comment