Mchango wa KKKT Dayosisi ya Karagwe katika maendeleo ya jamii.
Askofu
wa Dayosisi ya Karagwe Mh. Dr. Benson Bagonza akiwa na wageni
walioitembelea dayosisi toka Sweden mapema mwaka 2011 (Picha na KKKT DAYOSSISI
Dayosisi
ya Karagwe ni miongoni mwa dayosisi ishirini zinazounda Kanisa la
Kiinjili la Kilutheri Tanzania. Dayosisi ya Karagwe ilizinduliwa
rasmi tarehe 7/1/1979 pale Lukajange.
Tangu
wakati huo dayosisi ya Karagwe imeendelea kujihusisha na maisha ya
jamii ya wana Karagwe kwa kutoa huduma za kijamii na kuendesha shughuli
za maendeleo katika wilaya za Karagwe na Ngara. Huduma zote zinazotolewa
na Dayosisi ya Karagwe huwalenga wanajamii wote bila kujali dini zao,
kabila wala rangi zao.
Zifuatazo ni huduma za maendeleo ambazo hutolewa na Dayosisi ya Karagwe.
1. Huduma
za Afya-
Dayosisi ya Karagwe inamiliki Hospitali ya Nyakahanga ambayo
ndiyo hospitali teule ya wilaya ya Karagwe.Hospitali hii ni mkombozi kwa
jamii ya watu wa Karagwe na maeneo jirani kama wilaya mpya ya Misenye.
Huduma za kinga na tiba hutolewa katika hospitali hii.Pia hutoa huduma
nyingine kama huduma ya afya ya msingi, upimaji wa virusi vya Ukimwi kwa
hiari (ANGAZA), kliniki kwa ajili ya akina mama waja wazito nk. Pia
hospitali ya Nyakahanga inaendesha na kusimamia zahanati nyingine nne
ambazo ni Nyakatera, Ibamba-Mabira, zahanati ya shule ya sekondari
Karagwe na Katenga-Ngara.
2. Mradi
wa kudhibiti Ukimwi-
Kutokana na janga la ugonjwa wa Ukimwi unaowatesa
watu wengi, dayosisi ya Karagwe iliamua kuanzisha mradi huu ili
kuwasaidia watu katika jamii ya Karagwe kwa kuwapatia elimu juu Ukimwi,
kusaidia yatima hasa kuwalipia karo na mahitaji mengine kwa kusaidiana
na familia, kutoa chakula kwa wanaoishi na VVU pamoja na mambo ya haki
na utetezi hasa kwa wajane ambao kwa njia moja au nyingine huwa katika
hatari ya kukosa haki zao katika familia za waume zao.
3. Udiakonia
na utetezi-
Dayosisi ya Karagwe inawajibika katika kufanya shughuli za
diakonia ikiwa ni kuwasaidia wasijiweza au watu ambao wanaishi katika
mazingira hatarishi. Hapa makundi ya watu kama wazee, walemavu, wenye
mtindio wa akili, nk husaidiwa katika kupatiwa mahitaji ya lazima
ikiwemo chakula, mavazi, kuwajengea nyumba, kuwanunulia mashamba na
kuwatetea wale walio katika hatari ya kukosa haki zao.Vilevile kitengo
cha diakonia hutoa msaada wa mbuzi watano kwa kila familia
iliyobainishwa kuwa maskini ili kwa njia hiyo mradi huo wa mbuzi
uwasaidie kuongeza kipato cha familia ili waweze kujipatia mahitaji ya
msingi pale nyumbani. Pia kitengo hiki cha diakonia hutoa elimu kwa
jamii ili ione umuhimu na wajibu katika kuwasaidia wenye shida maana
wanaishi nao katia jamii moja.
4. Elimu-
Hii pia ni sehemu muhimu ya kazi ya dayosisi ya Karagwe. Mpaka sasa
dayosisi ya Karagwe inamiliki shule mbili za Sekondari ambazo ni Shule
ya Sekondari Karagwe (KARASECO) na Shule ya Sekondari ya wasichana
Bweranyamge. Katika matokeo ya mtihani wa kidato cha nne mwaka 2010
KARASECO imeshika nafasi ya pili (2) kimkoa kati ya shule 155 zenye
idadi ya wanafunzi zaidi ya arobaini na ya 44 kitaifa kati ya shule
3196. Bweranyange imeshika nafasi 4 kimkoa kati ya shule 32 zenye
wanafunzi chini ya 40 na ya 64 kitaifa kati ya shule 490. Pia dayosisi
inamiliki shule mbili za kiingereza ambazo ni Tegemeo (English Medium)
na Imani (English Medium). Vituo vingine vya elimu ni kama ifuatavyo:
Chuo cha Biblia Nkwenda, Chuo cha ufundi na kilimo Nkwenda, Chuo cha
ufundi staid kwa watoto yatima Lukajange, Chuo cha udiakonia na waalimu
wa shule za awali Nkwenda. Pia katika upande wa elimu,dayosisi ya
Karagwe inao mpango maalumu wa kuanzisha chuo kikuu hapa Karagwe na
mipango inaendelea vizuri kwa matumaini kwamba chuo hiki kitaweza kuanza
kupokea wanafunzi mwaka 2013 kama mipango yote itaenda kama
ilivyopangwa.Ikumbukwe kwamba huduma zote za elimu hutolewa kwa watu
wote bila kujali dini wala kabila.
5. Miradi
ya Maendeleo:
Dayosisi pia inasimamia miradi ya maendeleo kwa ajili ya
jamii ya Karagwe na watu wengine wote kama ifuatavyo:Karagwe Hotel and
guest house: Hiki ni kituo ambacho hutoa huduma za malazi chakula na
ukumbi wa mikutano. Watu mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi
hufurahia kutumia kituo hiki kwa sababu ya huduma zake bora, uaminifu wa
wahudumu na utulivu uliop sehemu hiyo. Unafuu wa bei pia huwavutia
watumiaji maana bei zetu zinalenga huduma zaidi kuliko biashara. Miradi
mingine ni kama mashine za kusaga nafaka huko majimboni, miradi ya
maji, upandaji miti, uwanja wa Ndege Ihanda, miradi ya wanawake ya
kuinua kipato chao kama ufugaji wa kuku, ushonaji nk
Baadhi ya wanafunzi wa shule ya sekondari ya wasichana BweranyangeDayosisi ya Karagwe (Picha na Mchg.Oscar Samwel
6. Mradi
wa utunzaji wa mazingira:
Dayosisi ya Karagwe iko mstari wa mbele
katika kutunza mazingira kwa kuamini kwamba mazingira ni uhai. Mradi huu
unahusisha majimbo yote, sharika na mitaa ambapo inasisitizwa kwamba
maeneo yote ya Kanisa yapandwe miti. Kwa mfano: Mwaka 2011 katika
majimbo ya Mabira, Murongo, Bweranyange na Kyerwa jumla ya miti 500.000
ilipandwa chini ya mradi huu ambao uliazishwa mwaka 2004. Katika
harakati hizi za utunzaji mazingira, dayosisi ya Karagwe kwa
kushirikiana na Jimbo rafiki huko Ujerumani imeanzisha mradi wa
mazingira uitwao KAKAUMAKI (Kampeni Kabambe ya Utunzaji mazingira
Kituntu). Mradi huu unatekelezwa katika Jimbo la Kituntu na kwa mwaka
jana jumla ya miti 17,500 ilipandwa. Pia dayosisi ya Karagwe inahimiza
vituo vyake vyote ikiwemo mashule na vituo vingine kuhakikisha wanapanda
miti kwa wingi ambayo mbali na kutunza mazingira lakini pia huko mbele
ya safari itakuwa kitegauchumi pindi itakapovunwa.
7. Mradi
wa Maisha mapya (New life in Karagwe)
PICHA TOKA MAKTABA YA KARAGWE ALBUM
Huu ni mradi ambao ulianzishwa
mwaka 2006 na unalenga kuwawezesha wanajamii kubadili maisha yao toka
hali duni ya kipato hadi kupata hali nzuri na kumudu kutunza familia
zao. Mradi huu unahusika na kuwasaidia wakulima waweze kulima kwa
kutumia mbinu za kisasa ambapo mkulima hupewa Ng’ombe mmoja jike ili
pamoja na kupata maziwa lakini pia mkulima hupata mbolea kwa ajili ya
shamba lake na hivyo kipato cha familia kuongezeka. Upande wa wanawake
wajane wao hupewa mbuzi wa maziwa. Mpaka sasa jumla ya Ng’ombe 300 na
mbuzi 100 tayari wamegawiwa kwa walengwa. Pia semina hutolewa kwa
wakulima jinsi ya kulima kwa tija na kutunza mazingira. Wakulima hupata
nafasi ya kutembelea maeneo ya kilimo ili kujifunza kwa vitendo.Mfano
mwaka 2010 wakulima walitembelea Maruku Bukoba na Igabiro ambapo
walipata nafasi ya kujifunza kwa vitendo. Kadhalika mradi huu
unawaelimisha watu juu ya utunzaji mazingira
8. Mradi
wa kujengea uwezo watoto wa kike (wasichana):
Mradi huu ni kwa ajili ya
kuwasaidia wasichana walio katika umri mdogo vijijini na hata mashuleni
ili waweze kujitambua na kujikinga dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi, ubakaji
nk. Pia hufundishwa na kuelekezwa juu ya haki zao za msingi ili waweze
kujitetea mbele ya jamii. Mbali na hayo pia mradi huu unalenga kuwabaini
wasichana ambao kwa sababu za umaskini wa familia zao wameshindwa
kuingia sekondari kwa kukosa karo. Wakishabainiwa mradi unawasaidia
kuwalipia karo na mahitaji ya shule, mpango huu utaanza rasmi mwaka huu.
9. SACCOS:
Huu ni mpango wa kuwasaidia wananchi ili waweze kuweka na kukopa
kupitia vikundi vyao vya SACCOS ambao ulianza rasmi mwaka 2009. Mpaka
sasa jumla ya Saccos 8 tayari zimesajiliwa katika majimbo ya Ihembe na
Bweranyange. Kitengo cha Saccos ambaocho kiko makao makuu ya dayosisi
Lukajange huwasaidia wanachama kuwapatia elimu kwa njia ya semina,
kuwapa vitendea kazi hasa wakati wa kuanza kama vitabu, kasiki, nk. Pia
kwa sasa wako katika kuziwezesha Saccos hizo kujenga ofisi za kuduma
ambapo kikundi husaidiwa kupewa mabati, sementi, milango na madirisha ya
chuma,vifaa vingine ni mchango wa wanachama.
No comments:
Post a Comment